Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Kigamboni, Dar es Salaam - Maulana Sheikh Hemed Jalala Mwakindenge amesema kuwa Uislamu wa kweli ni Uislamu wa ushindi, utukufu na mshikamano, unaojengwa juu ya mafundisho ya Karbala na imani ya kungojea kuenezwa kwa haki na Uadilifu katika Ardhi kupitia Imam wa Zama, Imam Mahdi (atfs).
Sheikh Jalala aliyasema hayo katika hotuba yake kwenye hafla ya kuadhimisha kuzaliwa kwa Imam Mahdi (atfs) pamoja na kumbukumbu ya miaka 47 ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, iliyofanyika leo katika Ukumbi wa Jamiatul Mustwafa, Kigamboni.
Aya ya Ushindi
Katika hotuba yake, alianza kwa kusoma Aya Tukufu ya Qur’an inayosema:
"كَتَبَ اللَّهُ لَأَغْلِبَنَّ أَنَا وَرُسُلِي إِنَّ اللَّهَ قَوِيٌّ عَزِيزٌ"
(Hakika Mwenyezi Mungu ameandika: Bila shaka Mimi na Mitume wangu tutashinda. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye izza).
Baada ya kusoma Aya hiyo, Sheikh Jalala aliwapongeza waumini kwa kuadhimisha mazazi ya Sahibul-Asr waz-Zaman, Imam Mahdi (atfs), na pia kuhuisha kumbukumbu ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yaliyoasisiwa na Imam Ruhullah Khomeini (RA).
Siri za Ushindi wa Kiislamu
Akifafanua Aya hiyo, Sheikh Jalala alisema kuwa Uislamu una siri kadhaa za ushindi, mojawapo ikiwa ni kuishi kwa vitendo mafunzo ya Imam Hussein (a.s) aliyoyasimamia katika ardhi ya Karbala.
“Siri ya pili ni kuamini uwepo wa Imam wa Zama, Sahibul-Asr waz-Zaman, Imam Mahdi (atfs), ambaye ndiye matumaini ya haki na uadilifu duniani,” alisema.
Aliongeza kuwa uwepo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni sehemu ya ushindi wa Uislamu, kwa kuwa ni dola inayotetea Uislamu wa hekima na uongozi wa kweli ulioasisiwa na Imam Khomeini (RA) na kuendelezwa na Kiongozi wa Mapinduzi, Sayyid Ali Khamenei (Allah Amuhifadhi).
Uislamu wa Karbala, sio wa Udhalili
Sheikh Jalala alisisitiza kuwa Uislamu si dini ya udhalili bali ni dini ya heshima, akirejea kauli ya Imam Hussein (a.s):
"هيهات منا الذلة"
"Haiwezekani sisi kukubali udhalili".
Alifafanua kuwa Uislamu unakataa kunyenyekea mbele ya madhalimu na huchagua maisha ya heshima, ujasiri na kupambana na dhulma kwa misingi ya haki.
“Uislamu una siasa ya Karbala. Na huo ndio Uislamu unaotambua adui, na kupambana naye, na kuhakikisha haki na uadilifu vinatawala duniani,” alisema.
Uongozi na Mustakabali wa Umma
Kwa mujibu wa Sheikh Jalala, nguvu ya Uislamu inatokana na uwepo wa uongozi, wanazuoni, marjaa, na Naibu wa Imam wa Zama, Sayyid Ali Khamenei, ambao huutuliza Umma hata katika nyakati ngumu na kuwapa matumaini ya ushindi.
“Uislamu hautetereki kwa sababu una itikadi kwamba dhulma itaondoka na haki itatawala. Uislamu ni ushindi, izza na utukufu,” aliongeza.
Mahudhurio ya Viongozi wa Dini
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Masheikh mbalimbali wakiongozwa na Mwenyekiti wa Jumuia ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), Dr. Sheikh Al-Had Mussa Salum, pamoja na waumini kutoka maeneo tofauti ya Dar es Salaam.
Sheikh Jalala alihitimisha kwa kuwataka Waislamu kushikamana na Uislamu halisi wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) na kuishi na thaqafa ya Karbala ya Imam Hussein (a.s) ili Umma uendelee kusonga mbele kwa heshima na nguvu.
Your Comment